Lugha za Kibantu
From Wikipedia
Lugha za Kibantu ni kundi la lugha ambalo liko tawi moja la lugha za Niger-Congo. Lugha za Kibantu huzungumzwa katika nchi za Kamerun, Nigeria, Gabon, Guinea ya Ikweta, Kongo zote mbili, Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya, Tanzania, Angola, Zambia, Malawi, Msumbiji, Zimbabwe, Namibia, Botswana, na Afrika ya Kusini. Enezi hilo linaonyesha kwamba kundi la lugha za Kibantu ni kubwa kabisa barani mwa Afrika, na idadi ya wasemaji Wabantu ni takriban milioni 310.
Neno la Bantu, maana yake ni watu katika lugha nyingi za Kibantu. Shina lake ni -ntu, na kiambishi awali cha ba- kinaonyesha uwingi. Kwa sababu hiyo, mtaalamu Wilhelm Heinrich Immanuel Bleek (aliyeishi 1827 hadi 1875) alitumia neno la Bantu kwa kurejea kundi la lugha hizo. Bleek alilinganisha sarufi za lugha mbalimbali za Kibantu, na baadaye Carl Meinhof alimfuata katika utafiti huo.
Kuna mamia ya lugha za Kibantu; wataalamu wengine wanahesabu 300, wengine wanahesabu 600. Mtaalamu Malcolm Guthrie aliziainisha kulingana na maeneo ya kijiografia. Kila eneo limepata herufi yake—A, B, C, D, E, F, G, H, K, L, M, N, P, R na S—na ndani ya kila eneo kuna tarakimu tena. Pia, Guthrie alichunguza lugha ya nasaba ambayo ni chanzo cha lugha zote za Kibantu.
[edit] Lugha za Kibantu zenye wasemaji wengi
(Idadi ya wasemaji ni makadirio tu; bado zinatofautiana kati ya makala na makala)
- Kiswahili na lahaja zake (wasemaji milioni 35) : Tanzania, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Komori, Mayotte, Msumbiji, Somalia.
- Kinyarwanda-Kirundi : (wasemaji milioni 15): Rwanda, Burundi
- Lingala (wasemaji milioni 10): Angola, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Gabon
- Chichewa (wasemaji milioni 9) : Malawi
- Zulu (wasemaji milioni 9) : Afrika Kusini
- Shona (wasemaji milioni 7) : Msumbiji, Zambia, Zimbabwe
- Kikongo (wasemaji milioni 6) : Angola, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
- Chiluba (wasemaji milioni 6) : Jamhuri ya Kidemocrasia ya Kongo, Angola
- Gikuyu (wasemaji milioni 4,6) : Kenya