Delta
From Wikipedia
Delta ni jina kwa ajili ya mdomo wa mto ukiwa na umbo la la kufanana herufi ya Kigiriki Δ (=delta) sawa na pembetatu.
[edit] Kutokea kwa delta ya mto
Umbo hili hutokea kama maji ya mto yanabeba matope, mchanga na mashapo mengine hadi mdomo wake baharini. Maji ya mto yakiingia baharini hupungua mwendo wake pia nguvu ya kubeba yaliyomo ndani yake. Mashapo yanashuka chini: kwanza sehemu zake nzito nzito kama changarawe, halafu mchanga, halafu udongo. Mashapo haya yanalazwa ganda baada ya ganda na kuimarika hadi kuonekana juu ya uwiano wa maji. Sehemu hizi za mashapo yaliyoimarika zinakuwa kama kizuizi kinacholazimisha mto kugawa mwendo wake. Kwa njia hii mikono mbalimbali inatokea. Mimea inaanza kukua kwenye nchi mpya ikiwa mizizi yao inashika na kuimarisha nchi hii.
Mto unaendelea kupeleka mishapo yake mdomoni na kujenga delta yake ndani ya bahari jinsi inavyoonekana kwenye mto Nile ambako delta imetoka nje ya mstari wa pwani.
Ikiwa bahari ina tofauti kubwa kati ya maji kujaa na kupwa mdomoni wa mto tena bahari haina kina kubwa hutokea mlango wa mto mwenye umbo la V (kama faneli) kwa sababu mwendo wa maji kujaa na kupwa unazuia kutelemka na kuimarika kwa mashapo.
[edit] Mito mikubwa yenye mdomo wa delta
Pamoja na mto Nile kuna mito mingi mikubwa yenye mdomo wa delta:
- mto Niger katika Nigeria
- mto Zambezi katika Msumbiji
- Amerika kuna delta za Amazonas (Brazil) na Mississippi (Marekani)
- Asia ina delta kubwa za Tigris-Euphrates (Irak), Indus (Pakistan), Ganga/Brahmaputra (India na Bangladesh), Krishna-Godavari na Kaveri (India), Ayeyarwady (Myanmar), Mekong (Vietnam) na Yangtse (Uchina).
- Ulaya kuna delta kubwa za Rhine (Uholanzi), Rhone (Ufaransa), Danubi (Romania), Ebro (Hispania), Volga na Lena (Urusi)
[edit] Delta ya barani
Wakati mwingine delta inatokea barani pasipo na bahari. Kuna hasa aina mbili: ama mto unakwisha barani (hasa kama ni jangwa) au mto unaendelea.
Huko Mali kuna delta ya barani ya mto Niger; mto unajigawa kwa mikono mbalimbali katika eneo kubwa la maziwa na maeneo ya matopematope.
Mto wa Okavango unakwisha kwenye delta yake katika jangwa la Kalahari (Botswana). Delta hii ni eneo lenye mimea na wanyama wengi katikati ya jangwa kubwa. Delta inavuta watalii wengi kila mwaka.