Mahakama
From Wikipedia
Mahakama ni chombo maalum chenye madaraka kisheria ya kutoa haki, kusuluhisha migogoro ya kiutawala, kikazi, na kutafsiri sheria na katiba katika nchi. Katika nchi zilizotawaliwa na Uingereza, mahakama ndio chombo kikuu cha kutoa haki na kusuluhisha migogoro. Kila raia katika nchi huwa na haki ya kupeleka madai katika mahakama zinazohusika na wale walioshtakiwa huwa na haki ya kujitetea mbele ya hakimu au jaji. Kawaida mshtakiwa yoyote yule huchukuliwa kuwa hana hatia hadi pale mahakama itakapoamua kuwa mtu huyo ana hatia. Hii ni moja ya kanuni kuu za kisheria.
Baadhi ya mifumo ya sheria huwa na mahakama ambazo hufanya kazi pamoja na hakimu/jaji na baraza la wananchi ambalo ndio hutoa uamuzi chini ya hakimu au jaji. Marekani ni kati ya nchi zenye mfumo huu. Nchi nyingine zina mahakama ambazo maamuzi yake hutolewa na jaji au hakimu tu.
Kwakuwa kuna mahakama za aina mbalimbali na zenye uwezo tofauti, uamuzi kuhusu mahakama ipi ina mamlaka gani hutokana na vifungu vya sheria au katiba.