Tripoli (Libya)
From Wikipedia
Kwa miji mingine inayoitwa "Tripoli" tazama makala ya maana Tripoli
Tripoli ni mji mkuu wa Libya. Jina la Kiarabu ni طرابلس (tarāblus) au طرابلس الغربية (tarābulus al-gharbiyya - Tripoli ya Magharibi kwa sababu ya Tripoli ya mashariki huko Lebanon) lina asili ya lugha ya Kigiriki (Τρίπολη) la kumaanisha "miji mitatu".
Tripoli ina wakazi 1,150,990 ambayo ni zaidi ya robo moja ya wakazi wote wa Libya na huku ikiendelea kukua haraka. Mji uko ufukoni mwa Mediteranea ikiwa na hali ya hewa ya wastani. Mwezi Agosti inafika halijoto ya sentigredi 28,1, Januari sentigredi 12,1°. Miezi ya baridi kuna mvua, Juni hadi Agosti hakuna mvua kabisa.
Tripoli ina bandari kubwa kabisa ya Libya na pia ni kitovu cha serikali, biashara na viwanda.
Tripoli ni mji wa kale ambao bado historia yake imetunzwa ikionyesha mabaki ya historia yake ndefu tangu enzi za Wafinisia, Waroma, Waarabu, Wahispania, Waturuki na Waitalia.